Dar es Salaam. Hilo ndilo jeshi jipya la Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Ndivyo unavyoweza kuliita.

Ni jeshi linalokuja kukabiliana na hoja za vyama vya upinzani vilivyoruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara, baada ya kuzuiwa kwa takribani miaka sita mfululizo.

Ni kipindi ambacho Watanzania wanataka kusikia kauli za matumaini kwa chama hicho, kuhusu hali ngumu ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha ambapo kuanza kwa mikutano ya hadhara kutaibuka hoja mbalimbali zikiwamo za mambo yanayowagusa moja kwa moja wananchi.

Ni kama CCM imeliona hilo na sasa imeunda sekretarieti mpya ya kupambana na hoja za upinzani.

Awali Rais Samia aliwaeleza wanachama wa CCM, kukaa sawa kujibu kwa hoja si kupayuka hoja zitazokuwa zikiibuliwa na wapinzani.

Mabadiliko hayo ya yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kilichoketi chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia ambapo pamoja na mambo mengine kiliteua sekretarieti mpya ya chama hicho na kujaza nafasi saba za Kamati Kuu.

Katika sekretarieti hiyo iliyotangazwa yenye wajumbe saba, waliosailia kutoka ya awali ni wawili pekee ambao ni Katibu Mkuu, Daniel Chongolo pamoja na Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha, Dk Frank Hawasi.

Mabadiliko hayo yalitangazwa jana ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam na Shaka Hamdu Shaka ambaye nafasi yake ya uenezi imechukuliwa na Sophia Mjema ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Shaka aliwataja pia manaibu Katibu wawili, akiwamo Annamringi Macha (Naibu Katibu Mkuu Bara) aliyechukua nafasi ya Christina Mndeme.

Macha amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Pia, amewahi kuwa katibu msaidizi wa CCM kuanzia ngazi za wilaya na baadaye mkoa. Akaja kuwa katibu msaidizi mkuu idara ya uenezi.

Shaka ambaye anabaki na nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu alisema, Mohamed Said Dimwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar akichukua nafasi ya Dk Abdallah Juma Sadalla.

Pia, Mbarouk Nassor Mborouk ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ye Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameteuliwa kuwa Katibu ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa akichukua nafasi ya Kanali mstaafu Ngemela Lubinga

Mwingine ni Issa Haji Ussi ‘Gavu’ aliyeteuliwa kuwa Katibu wa NEC Idara ya Oganaizesheni akichukua nafasi ya Mauldine Castico.

Awali, Shaka alisema uteuzi wa kwanza ulikuwa ni wa kuziba nafasi saba za Kamati kuu, ambapo walioteuliwa ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, Hassan Wakasovi aambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora na Halima Mamuya (aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa UWT).

Kwa upande wa Zanzibar, walioteuliwa kuziba nafasi hizo ni pamoja na Mohamed Aboud Mohamed, Mhandisi Nasir Ally (mjumbe wa NEC) na Leyla Burhan Ngozi.

Mabadiliko hayo yamekuja ukiwa umepita mwezi mmoja tangu CCM ilipofanya mkutano mkuu jijini Dodoma uliohitimisha uchaguzi wa ndani wa chama hicho ikiwa pamoja na kuchagua viongozi wakuu akiwemo Mwenyekiti Rais Samia na Makamu wake, Abdulrahman Kinana (Bara) na Rais Hussein Mwinyi (Zanzibar).

Katika uchaguzi huo, Shaka aligombea na kushinda nafasi ya ujumbe wa NEC sawa na Sadalla ambao kwa sasa wameondolewa kwenye sekretarieti.

Mabadiliko hayo yamekuja wakati tayari Rais Samia ameshatangaza kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, ambapo amewataka viongozi na makada wa chama hicho kuwa tayari kujibu hoja za vyama vya upinzani.


 
Top