Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Ndugu Sophia Mjema amesema wanaCCM wote nchini wanalo jukumu la kuelewa sera, itikadi za CCM na miradi ya Serikali inayotekelezwa na Serikali ya CCM na kuieneza kwa Watanzania wote bila kigugumizi chochote kile. Mjema ameyasema hayo leo Machi 01, 2023 kwenye mwendelezo wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo na Sekretarieti yake kwenye mkoa wa Singida akiwa kwenye tawi na 6 lililopo kijiji cha Ulemo kata ya Ulemo Wilayani Iramba kwenye mkutano wa tawi. "WanaCCM tusiwe na kigugumizi katika kusemea sera, itikadi ya CCM pamoja na miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya CCM na kuieneza kwa wananchi ili waelewe kazi kubwa inayofanywa. Tusiposema sisi wanaCCM namna sera zetu zinavyotatua changamoto za huduma za kijamii na kuimarisha miundombinu basi watakuja wengine kusema kwa namna isiyo nzuri." Alisema Mjema. "WanaCCM tuelewe itikadi ya CCM ya ujamaa na kujitegemea na sera zetu nzuri zinazoshusha maendeleo makubwa na kueneza Chama chetu kwa wananchi. Kazi ya MwanaCCM ni kueneza na kutetea kazi kubwa hii inayofanywa kwenye nchi yetu na wanaCCM tutambe mbele za watu tukieleza haya bila kuwa na kigugumizi chochote kile." Alisisitiza Mwenezi Mjema amesisitiza kwamba CCM itaendelea kushusha elimu ya sera zake, itikadi yake pamoja na miradi mikubwa inayotekelezwa kwa Viongozi wake wapya waliochaguliwa hivi karibuni ili wawe na uelewa nazo ili waweze kuzieneza na kuzinadi kwa Watanzania nchi nzima sababu CCM ndiyo Chama tawala na hivyo ni lazima wananchi waelewe uelekeo wa Chama hiki.

 
Top